Dar es Salaam: Watatu kizimbani kwa tuhuma za uhujumu uchumi

0
275

Watu watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matano likiwemo kosa la uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha, Dola za Marekani zaidi ya 300,000, mali ya Kampuni ya SMCI ya Marekani.

Washitakiwa hao Deogratias Masika, William Kimonge, wakazi wa Dar es Salaam na Youssouf Sabo, raia wa Cameroon wamesomewa shitaka lao mbele ya Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo Cassian Matembele.

Wakili wa Serikali, Annastazia Willson amedai kuwa washitakiwa hao kati ya Decemba 2016 na Januari 2017 jijini Dar es Salaam walilaghai Kampuni ya SMCI ya Marekani na kujipatia Dola za Marekani 320,000 wakidanganya kuwa wataisambazia kampuni hiyo tani 5,000 za korosho kutoka Mtwara wakati sio kweli.

Katika shitaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, washitakiwa hao wanadaiwa kuilaghai Kampuni ya SMCI ya nchini Marekani na kujipatia Dola za Marekani 15,000 wakidanganya kuwa wataisambazia kampuni hiyo tani 10,000 za korosho kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam wakati sio kweli.

Aidha, washitakiwa hao wanadaiwa kuilaghai kampuni tajwa na kujipatia Dola za Marekani zaidi ya 300,000 na kuziingiza kwenye akaunti ya CRDB yenye jina la JAW Distributors Limited kwa lengo la kubadilisha kuwa fedha za Kitanzania.

Hata hivyo washitakiwa hao wamekana shitaka linalowakabili huku Hakimu anayeendesha shauri hilo akidai dhamana ipo wazi kwa mshitakiwa namba mbili ambaye ametakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini Bondi ya milioni sitini na tisa kila mmoja.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septamba 29 mwaka huu na washitakiwa wote wamerudishwa Mahabusu.