Ndege ya abiria inayomilikiwa na Shirika la Lion Air la nchini Indonesia imeanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege mjini Jakarta ikiwa na watu 188.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737 – MAX 8 ilikuwa ikisafiri kutoka katika mji huo mkuu kwenda jiji la Pangkal Pinang lililopo kwenye visiwa vya Bangka Belitung.
Habari kutoka nchini Indonesia zinasema kuwa ndege hiyo ilitoweka kwenye mitambo ya rada dakika 13 baada ya kupaa ilipokuwa inavuka bahari.
Maafisa wa anga nchini Indonesia wamesema kuwa wakati ajali hiyo inatokea, ndege hiyo ambayo ni mpya ilikuwa imebeba abiria 181, marubani wawili na wahudumu watano.
Katika taarifa yake, shirika hilo la ndege la Lion Air ndege limesema kuwa chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo bado hakijajulikana na kwamba vyombo vya baharini viko katika eneo ilipotokea ajali hiyo.
Hadi sasa hakuna taarifa za mtu yeyote aliyenusurika katika ajali hiyo na jitihada za uokoaji zinaendelea.