Waombolezaji mbalimbali wakiwemo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamejitokeza kutoa pole nyumbani kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Jaji Mark Bomani aliyefariki jana Septemba 10, 2020.
Wakizungumzia marehemu Bomani, waombolezaji wamesema ameacha alama ya utumishi uliotukuka ndani na nje ya Tanzania hususani katika idara ya sheria.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Balozi Mstaafu Juma amesema marehemu ameugua kwa muda mrefu na kupata matibabu katika hospitali mbalimbali ndani na nje ya nchi hadi umauti ulipomkuta akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Aidha, baadhi waombolezaji na viongozi wa kisiasa wakiwemo Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema marehemu alikuwa mtu aliyezitumikia nchi za Namibia katika kurekebisha sheria zao huku akishika nafasi mbalimbali za uongozi
Mwili wa marehemu Jaji Bomani utazikwa Septemba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Bomani alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania kuanzia 1965 hadi 1976.