Sita kizimbani kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali ni silaha

0
181

Wafanyabiashara sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka tisa likiwemo kosa la kukutwa na nyara za serikali, vipande 24 vya meno ya tembo na silaha ya moto aina ya Riffle 458.

Wafanyabiashara hao ni Abdul Seif, Fauluna Matunday, Yusuf Rashid, Joseph Elio, Catherine Nanyinda na Abdallah Mwinyo.

Katika shitaka la kwanza, Wakili wa Serikali Candid Nasua amedai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Novemba 2019 na Augost 2020 washtakiwa hao wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu katika maeneo tofauti mkoani Lindi na jijini Dar es Salaam wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Shitaka la pili ambalo linawahusu mshitakiwa wa kwanza hadi wa tatu ni kumiliki na kusafirisha nyara za Serikali, vipande 24 vya meno ya tembo yenye thamani ya zaidi shilingi milioni 240 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Pia katika shauri hilo mshitakiwa namba nne ambaye ni Nanyinda anadaiwa kughushi kadi ya mpiga kura kinyume na sheria akionesha kadi hiyo ni halali wakati sio kweli.

Shitaka jingine ni la umiliki wa silaha ya moto aina ya Riffle 458 linalomkabili Mwinyo anayedaiwa kutenda kosa hilo kati ya 26 Agosti 2019 maeneo ya Mtawanga mkoani Lindi.

Baada ya kusoma hati ya mashitaka kwa washitakiwa hao, mwendesha mashitaka wa Serikali amesema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo ameiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi 22 Septemba, 2020 itakapotajwa.