Rais John Magufuli amekutana na wanunuzi wa zao la korosho na kutoa msimamo wa serikali kuhusu bei ya zao la korosho kufuatia kuwepo kwa mvutano wa bei ya zao hilo kati ya wanunuzi na wakulima.
Rais Magufuli amekutana na wanunuzi hao katika mkutano wa majadiliano uliokuwa ukiendelea kati ya wanunuzi hao wa korosho na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Katika msimamo huo Rais Magufuli amesema kuwa serikali inaungana na msimamo wa wakulima kukataa bei zilizotolewa na wanunuzi katika mnada uliofanyika hivi karibuni ambapo kampuni za ununuzi wa korosho zilitangaza kununua korosho kwa bei ya kati ya shilingi 2,717 na shilingi 1,900 kwa kilo ikiwa imeshuka kutoka zaidi ya shilingi 3,600 ya msimu uliopita.
Rais Magufuli amesema kuwa endapo wanunuzi hao hawatakuwa tayari kununua korosho kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kwa kilo, serikali ipo tayari kununua korosho kwa bei yenye maslahi kwa wakulima na kutafuta masoko yenye bei nzuri.
“Kama hamtanunua korosho kwa bei yenye maslahi kwa wakulima, serikali itanunua korosho kwa bei nzuri kwa wakulima na tutaihifadhi, nipo tayari hata kutumia majeshi yetu kununua korosho na tutatafuta masoko ya uhakika ili tuuze kwa bei nzuri” amesisitiza Rais Magufuli.
Wakizungumza katika mkutano huo, wanunuzi hao wa korosho wamekubali kununua korosho kwa bei isiyopungua shilingi 3,000 kama ilivyoelekezwa na serikali na wameomba baadhi ya tozo zinazosababisha kupungua kwa bei ya zoa hilo kwa mkulima ziondolewe pamoja na kuruhusiwa kusafirisha korosho kupitia bandari ya Dar es salaam ambako wanaweza kupata meli zinazotoza gharama nafuu za usafirishaji wa korosho kwenda kwenye masoko ya nje ya nchi.
Rais Magufuli amekubali kuondolewa kwa utozaji ushuru wa mara ya pili wa ushuru wa halmashauri uliokuwa ukifanywa baada ya korosho kufikishwa Mtwara, kupunguza ushuru wa Bodi ya Korosho Nchini kutoka shilingi 17 kwa kilo hadi shilingi 10 kwa kilo na ameruhusu wafanyabiashara kununua magunia yao wenyewe kwa ajili ya korosho badala ya kuuziwa na vyama vya ushirika kwa bei kubwa.
Kuhusu bandari ya kusafirishia korosho, Rais Magufuli amekubali ombi la wanunuzi hao wa korosho la kutaka kusafirisha korosho kwa kutumia bandari ya Dar es salaam ambapo kilo moja inasafirishwa kwa shilingi 47 kwa kilo kwa kutumia meli ambazo zimebeba mizigo mingine ikilinganishwa na bandari ya Mtwara ambako kilo moja inasafirishwa kwa shilingi 203 kilo kwa kutumia meli zinazokodiwa kwa ajili ya kubeba korosho tu.
“Bandari ya Mtwara na bandari ya Dar es salaam zote ni bandari za serikali, mimi sina tatizo na kusafirisha korosho kupitia bandari ya Dar es salaam, lakini na nyinyi muwe tayari kutozidisha uzito kwenye magari mnaposafirisha kutoka Mtwara hadi Dar es salaam, kutotorosha korosho na pia kutimiza masharti ya usafirishaji”, amesisitiza Rais Magufuli.
Ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha usafirishaji wa korosho hizo kupitia bandari ya Dar es salaam kama ambavyo wanunuzi hao wameomba.
Aidha, Rais Magufuli amewataka wanunuzi hao kuwekeza viwanda vya kubangua korosho ama kuwahamasisha washirika wao kuwekeza katika viwanda hivyo na kwamba serikali itaunga mkono juhudi hizo ikiwa ni pamoja na kuweka vivutio vya kodi.