Vipaumbele vya Prof. Lipumba akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania

0
245

Chama cha Wananchi (CUF) kimezindua kampeni leo shughuli iliyofanyika katika Uwanja wa Sabasaba mkoani Mtwara ikiwa ni hatua ya kuelekea Oktoba 28, 2020 siku ambayo wananchi watapiga kura kuchagua Rais, wabunge na madiwani.

Akizungumza katika mkutano huo, mgombea urais wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba amesema serikali yake itatekeleza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na:

Kuboresha sekta ya uvuvi na uchumi wa baharini, kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika kwa asilimia kubwa zaidi. Hii ni pamoja na kuongeza uwezo wa uvuaji samaki na upatikanaji wa soko la bidhaa hizo.

Pili, kuboresha kilimo kwa kuwekeza zaidi kwenye nafaka kwani tayari India imeihakikishia Tanzania soko la uhakika la nafaka zitakazolimwa nchini. Pia, ameahidi kuhakikisha soko la uhakika la korosho ambayo imekuwa ikiingiza fedha za kigeni.

Tatu, kuhakikisha wakazi wa mikoa ya kusini mwa Tanzania wananufaika na mradi wa gesi.

Nne, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na katiba mpya.

Tano, kuhakikisha elimu bora kwa watoto wote na kwamba kila mtoto anasoma kadiri ya uwezo wa akili yake na sio uwezo wa fedha za mzazi wake, na wanafunzi wanaanza kutumia kompyuta.

Sita, ameahidi kuboresha huduma za afya kwa wajawazito na watoto kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na akiba ya damu ya kutosha, lishe bora kwa watoto pamoja na matumizi ya teknolojia kutoa ushauri wa kitabibu kwa wagonjwa hata wale walio mbali na hospitali.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali yake itahakikisha kuna kuwepo na viwanda vya kutosha na maendeleo yatakayowagusa wananchi katika ngazi zote.