NEC yatupilia mbali mapingamizi dhidi ya Dkt. Magufuli na Prof. Lipumba

0
916

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa dhidi ya wagombea wa Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli na Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba.

Mapema leo mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu aliwasilisha mapingamizi hayo akidai kuwa wagombea hao hawakufuata kanuni na sheria za uchaguzi.

Lissu ameeleza kuwa Prof. Lipumba hakurudisha fomu za uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria. Pia, Lissu ameeleza kuwa Dkt. Magufuli hakuambatanisha picha kwenye fomu ya uteuzi na hakurudisha fomu kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria.

Akitoa uamuzi wa NEC, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Wilson Mahera amesema kuwa utetezi uliowasilishwa na wagombea hao umeidhihirishia tume kuwa mapingamizi hayo hayana msingi na yametupiliwa mbali.

Kufuatia uamuzi huo, Prof. Lipumba anaendelea kuwa mgombea halali kupitia CUF na Dkt. Magufuli anabaki kuwa mgombea halali kupitia CCM.