Rais Magufuli akagua magari yaliyotaifishwa, atoa maagizo

0
315

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli leo Agosti 25, 2020 amekagua magari yaliyotaifishwa baada ya kuhusika katika matukio ya uhujumu uchumi, na kisha kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani Jijini Dodoma.

Idadi ya magari hayo ni 130 yakiwemo makubwa na madogo yalikamatwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kisha wahusika kufikishwa mahakamani na mahakama kutoa uamuzi wa kuyataifa.

Akizungumza baada ya kuyakagua, Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Jeshi la Polisi na wote waliohusika kuwakamata waliokuwa wanajihusisha na vitendo hivyo (ikiwemo biashara haramu ya meno ya tembo) na ameagiza magari hayo yagawanywe katika taasisi mbalimbali za Serikali ili yatumike kuendesha shughuli za kuwahudumia wananchi na kuzalisha mali.

Rais Magufuli pia amewapongeza wananchi waliojitokeza kutoa taarifa zilizosaidia kukamatwa kwa watu waliokuwa wanafanya uhalifu kwa kutumia magari hayo na amewaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kukomesha vitendo hivyo.