Vyombo vya habari vyatakiwa kudumisha amani kuelekea uchaguzi

0
406
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na kufurahi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Olesanare wakati wa ziara ya kukagua usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuzungumza na Wadau wa Sekta ya Habari mkoani hapo Agosti 18, 2020.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amevitaka vyombo vya habari nchini kuendelea kudumisha na kulinda amani katika kipindi chote cha kampeni mpaka uchaguzi mkuu kwa kuandika na kutangazia umma habari ambazo zina ukweli.

“Mwanahabari ni mwalimu, mfasili, mkalimani, mchambuzi na mtetezi hivyo ni vizuri akatumia taaluma yake vizuri katika kuhabarisha umma ili asilete migogoro. Pia mwanahabari anapaswa kuelezea sera za wagombea na vyama vyao ili kuisaidia jamii kutambua mgombea sahihi na kuchagua mgombea bora,” amesema Mwakyembe.

Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa ifikapo mwaka 2021 hakuna Mwandishi wa Habari yeyote ambaye kama atakuwa hajakidhi vigezo vya Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake za mwaka 2017 ataruhusiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari, lengo likiwa ni kuifanya taaluma hiyo kutambulika na kuheshimika.