Wizara ya Kilimo yatakiwa kujitathmini

0
2207

Rais John Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini kutokana na suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea pamoja na utendaji wa Bodi ya Korosho Nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa pia ameiagiza Wizara ya Kilimo kumrudisha wizarani Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Nchini (CBT) Profesa Wakuru Magigi baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo katika kikao chake na wakuu wa mkoa inayolima zao la korosho kilichofanyika mkoani Lindi.

“Haturidhishwi na utendaji wa bodi ambao umekiuka maelekezo ya msingi ya Serikali katika kusimamia mfumo mzima wa zao la korosho uliopelekea kuvurugika kwa minada,” ameongeza Waziri Mkuu.

Kufuatia hali hiyo, amesema kuwa serikali imesitisha minada yote ya korosho nchini kuanzia Oktoba 26 na kuwataka wakulima wawe watulivu wakati suala hilo likishughulikiwa.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Korosho nchini analalamikiwa kwa kufanya kazi bila ya kushirikisha ushirika wa zao la korosho na kutotambua mamlaka zilizowekwa kisheria ikiwa ni pamoja mkuu wa mkoa.

Mbali na malalamiko hayo, Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Korosho Nchini pia anadaiwa kuendesha operesheni kwa kutumia silaha na askari dhidi ya viongozi wa ushirika kinyume cha taratibu za nchi.

Kutokana na malalamiko hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amewaagiza Makamanda wa Polisi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuhakikisha gari lenye namba T 814 DDM pamoja na dereva wake linatafutwa popote lilipo.

Waziri Mkuu amefafanua kuwa gari hilo ndilo linalodaiwa kutumika katika kuwakamata viongozi wa ushirika waliokuwa wanawasimamia wananchi waliokataa kuuza korosho kwa bei ndogo.

Amesisitiza kuwa baada ya dereva wa gari hilo kukamatwa ahojiwe na aeleze askari hao alikuwa anawatoa wapi na nani aliyemtuma na kwamba askari wote waliohusika watafutwe.

“Bodi imekuwa ikiwatisha na kuwalazimisha wakulima na viongozi wa ushirika kukubali kuuza korosho kwa bei ya chini jambo ambalo Serikali haiwezi kulikubali,” amesema Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo kwa sababu limekuwa likiipaka matope kwa kuwa Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Korosho Nchini alikua akiingiza askari katika mikoa hiyo bila ya mamlaka kuwa na taarifa.

Kadhalika Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo kutokaa kimya pindi zinapotokea changamoto kama hizo na badala yake watoe taarifa mapema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Rais John Magufuli amewapongeza wakulima wa korosho kwa uamuzi wao wa kukataa kuuza korosho kwa bei ndogo na kwamba yuko pamoja nao.

“Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini katika suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea,” amesema Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Magufuli ana taarifa kwamba kuna baadhi ya watendaji serikalini wanatumia vibaya jina lake na kwamba ni lazima wahusika wote watachukuliwa hatua.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, – Gelasius Byakanwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi, – Godfrey Zambi walilalamikia kitendo cha Profesa Magigi kuvuruga mfumo wa uuzaji wa korosho.

Pia walisema licha ya kumshauri kiongozi huyo juu ya namna bora ya kuendesha minada ya uuzaji wa korosho hakuwasikiliza na kwamba hakuwa tayari kushirikiana nao na pia alikuwa akidharau mamlaka zao.

Pia alikuwa akiingiza askari na kuwatisha na kukamata viongozi wa ushirika bila ya wao kujua jambo ambalo walisema limezua taharuki kwa watendaji wa ushirika.