Serikali ya Jimbo la Hunan imeanzisha mtaa maalum wa kuuza kahawa kutoka Barani Afrika katika soko kuu la Gaoquiao jijini Changsha.
Hafla ya uzinduzi wa mtaa huo umefanyika jana na kuhudhuriwa na wawakilishi wa mataifa mawili, Tanzania na Ethiopia yanayozalisha kahawa.
Hunan Galquiao Grand Market ni soko la tatu kwa ukubwa nchini China linalouza bidhaa mbalimbali kutoka ndani na nje ya China.
Uzinduzi wa mtaa wa kuuza kahawa kutoka Afrika ni sehemu ya hatua za Jimbo la Hunan kufungua soko lake kwa bidhaa kutoka barani Afrika.
Hafla ya ufunguzi wa mtaa wa kahawa ilifuatiwa na mkutano wa biashara uliohudhuriwa na washiriki 360 (onsite) na 2000 (online) ambapo nchi za Tanzania, Ghana na Ethiopia zilipata fursa ya kuwasilisha mada juu ya fursa za biashara ya mazao ya kilimo na uwekezaji katika viwanda.
Balozi wa Tanzania, Mbelwa Kairuki ameyakaribisha makampuni ya Jimbo la Hunan kuwekeza nchini Tanzania kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo yanayolimwa Tanzania ikiwa ni pamoja na korosho, pamba, katani, ufuta, muhogo, karanga na soya.