Meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu kuanza safari

0
361

Meli ya New Victoria-Hapa Kazi Tu itaanza kutoa huduma za usafirishaji kati ya Mwanza na Bukoba Jumapili Agosti 16, baada ya ukarabati na vibali vyote vinavyohitajika kwa meli hiyo kuanza kazi kukamilika.

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Huduma za Meli nchini, Erick Hamis, ametangaza ratiba ya meli hiyo kuanza kutoa huduma kufuatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwishoni mwa juma lililopita ambapo aliagiza mamlaka zinazohusika kutoa vibali ili meli hiyo ianze kutoa huduma.

Kufuatia agizo hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Huduma za meli nchini Erick Hamis, amekutana na waandishi wa habari jijini Mwanza na kutangaza ratiba ya safari za meli ambazo zitaanza safari Jumapili ijayo ya Agosti 16.

Huduma ya usafiri wa meli kati ya Mwanza na Bukoba inarejea baada ya kukosekana kwa mika sita, huku serikali ya awamu ya tano ikiwa na mpango wa kuongeza meli nyingine saba, na kufikisha idadi ya meli 22 kutoka 15 zilizopo hivi sasa.

Meli hizo za New Victoria-Hapa Kazi Tu na New Butiama-Hapa Kazi Tu zimekarabatiwa kwa teknolojia ya kisasa kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 26, zina injini mpya za teknolojia ya kisasa na mwonekano wa kisasa kwa ndani.