Viongozi wa siasa wameaswa kuwa makini na kauli zao ili kukwepa kutoa matamshi yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Mwezi Oktoba mwaka huu.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzina katika kipindi cha Jambo kinachorushwa na TBC ambapo amesema viongozi wa dini wakichunga kauli zao itakuwa rahisi kuwaongoza waumini wao katika miongozo ya amani na utulivu ili kuleta mustakabali mzuri kwa taifa.
Amesema kauli za uchochezi haziwajengei umaarufu viongozi wa kisiasa na badala yake hulitumbukiza taifa husika katika machafuko, suala ambalo Watanzania wanapashwa kuliepuka kwani tayari taifa limesimama katika dira ya kujiletea maendeleo.
Aidha, Askofu Gwajima amewataka waumini wa dini kubadilika kutoka kutenda maovu na kutenda mema hatua ambayo itasaidia kujenga jamii yenye hofu na Mungu na kutii mamlaka zilizopo madarakani.