Mama Samia: Wanawake ndio wapigakura wa kuaminika

0
354

Makamu wa Rais, Samia Suluhu amewahakikisha wanawake kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika taifa, hivyo amewataka kutembea kifua mbele kwani wao ni jeshi kubwa.

Mama Samia amesema hayo wakati akizungumza na wanachama wanawake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Maalum kwa Uchaguzi ambao wamekutana kuchagua wabunge kupitia jumuiya hiyo.

“Tunatambua deni kubwa tulilonalo kwenu maana wanawake ndio waungaji mkono wakubwa wa Chama cha Mapinduzi wasiotetereka, wapigakura wa kuaminika na pia ndio walezi na watunzaji wa familia zetu,” amesema Mama Samia.

Ameongeza kuwa, kutokana na nafasi hiyo kubwa ya mwanamke, serikali inafanya linalowezekana kuwakomboa wanawake kielimu na kiuchumi.

Wakati huo huo, jumuiya hiyo imetoa cheti cha pongezi kwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa namna alivyoongoza mapambano dhini ya virusi vya corona.

“Waziri Ummy amefanya kazi ile akijua katika wizara ile anawakilisha kundi kubwa la wanawake,” amehitimisha Makamu wa Rais.