Waziri Jafo aweka wazi mafanikio yaliyopatikana kwenye elimu

0
298

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Selemani Jafo amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali imeongeza idadi ya shule za msingi na sekondari na kupelekea ongezeko kubwa la wanafunzi linalotokana na mfumo wa elimu bila malipo.

Ameeleza hayo katika maadhimisho ya siku ya elimu ya TAMISEMI inayoangazia mafanikio ya miaka mitano kwa upande wa elimu ambayo inajumuisha ongezeko la shule pamoja na ukarabati wa shule kongwe.

Awali, Waziri Jafo amekagua maonesho ya taasisi mbalimbali za elimu zilizoelezea mafanikio na ubunifu waliofanya ambapo pia ametembelea maabara za Shule ya Sekondari Dodoma na kupata maelezo kutoka kwa wanafunzi wanaofanya majaribio kwa vitendo kwenye maabara hizo.

Kuhusu ujenzi na/au ukarabati wa shule, Jafo ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano (2015/2020) kiasi cha shilingi bilioni 501.78 kimetumika kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Amesema katika kipindi hicho shule mpya za msingi 905 zimejengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, kuelekea uchaguzi mkuu, Waziri Jafo amesema Watanzania wanapaswa kuyalinda mafanikio yaliyopatikana kwa kufanya uchaguzi wa amani na kuendelea kudumisha utulivu uliopo nchini.

Amewasihi wasikubali kuharibu mafanikio yaliyopatikana nchini kwa kishawishiwa na watu wasio na nia njema na mafanikio yaliyopo.

Leo ni siku ya pili katika Wiki ya TAMISEMI ambapo wizara imeangazia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu.