Jeshi la Magereza Tanzania limeruhusu wananchi kutembelea wafungwa na mahabusu katika magereza mbalimbali na kuwapelekea vitu vinavyoruhusiwa ikiwemo vyakula.
Msemaji wa Jeshi la Magereza, Amina Kavirondo amesema kuwa uamuzi huo umetokana na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Zaidi ya miezi minne iliyopita jeshi hilo lilizuia utaratibu wa watu kwenda kuwatembelea wafungwa na mahabusu ukiwa ni mkakati wa serikali wa kudhibiti maambuziki ya virusi hivyo vilivyokuwa vimeingia nchini.
Licha ya kurejeshwa kwa utaratibu huo, amesema wageni watatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya wizara ya afya.
Utaratibu mpya unabainisha kuwa wafungwa na mahabusu, watatakiwa kutembelewa na ndugu wasiozidi wawili tu kati ya Jumamosi na Jumapili na mazungumzo yasizidi dakika tano.
“Wale wenye vibali vya kuwaletea chakula mahabusu italazimika kuletwa na mtu mmoja tu, na umbali wa mita moja kati ya mfungwa au mahabusu na mgeni ni lazima uzingatiwe,”amesema.
Wageni wanapaswa kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni wanapoingia eneo la gereza na wanapoingia gerezani, “lakini pia mazungumzo ya kisheria kati ya wakili na mteja wake hayatazidi saa moja,” amesema.