Elimu ya soko la mitaji yahitajika kwa Watanzania

0
2074

Mhitimu wa kozi ya utendaji katika soko la mitaji la viwango vya kimataifa Ahmed Masumai kutoka benki ya  CRDB amesema kuwa ataitumia elimu aliyoipata katika kuelimisha Watanzania namna ya kuunganishwa na soko la mitaji.

Masumai  ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam kando ya hafla ya kutoa zawadi kwa washindi wa shindano la  kuandika Insha, maswali  na majibu  kuhusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.

Ameongeza kuwa elimu aliyoipata itaongeza chachu ya uelewa kwa Watanzania wengi kuhusu masuala ya masoko, mitaji na dhamana, masuala ambayo Watanzania wengi hawayafahamu.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt  Philip Mpango ameishauri  Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Nchini (CMSA) kuendelea kutoa elimu na ujuzi kwa wanafunzi wa elimu ya juu kuhusu masoko ya mitaji ili waweze kuwa wawekezaji wa baadae katika biashara ya hisa.

Amesema kuwa elimu ya masoko ya mitaji kwa watanzania bado ipo chini,  hivyo elimu hiyo itasaidia kuongeza ujuzi na weledi wa kiwango cha kimataifa katika utendaji wa sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini.

Kwa upande wake afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, – Nicodemus Mkama amesema kuwa wameanza kuwashirikisha wanafunzi wote zaidi ya elfu 15  walioshiriki katika shindano hilo kwa kuwapatia elimu zaidi.

Amefafanua kuwa washiriki ishirini kati ya  washiriki hao zaidi ya elfu 15 wameibuka washindi ambapo mshindi wa kwanza amepata zawadi ya shilingi milioni moja na laki nane, mshindi wa pili shilingi milioni moja na laki nne,mshindi wa tatu ameibuka na shilingi laki nane na  mshindi wa nne amepata shilingi shilingi laki tano.

Kwa mujibu wa Mkama, washindi 12 kati ya ishirini watapatiwa ufadhili wa kimasomo nchini Mauritius, nchi inayofanya vizuri kwenye sekta ya masoko ya mitaji  ili kuongeza uwezo wa kiteknolojia katika sekta hiyo.

Shindano la kuandika Insha, maswali na majibu kuhusu masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini  lilikua na lengo la kupima uelewa wao katika masuala ya masoko ya mitaji na uwekezaji wa pamoja kwa kutumia njia za kielektroniki na lilifunguliwa Mei 22  na kufungwa Septemba 15 mwaka huu.