Ruben Loftuscheek ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Uingereza kuifungia Chelsea mabao matatu yaani Hat Trick katika mashindano ya vilabu Barani Ulaya tangu Septemba 29 mwaka 1971 pale Peter Osgood alipofunga mabao matano na Tommy Baldwin akiweka mengine matatu kwenye michuano ya kombe la washindi dhidi ya Jeunesse Hautcharage ya Luxemborg.
Loftuscheek amefunga mabao hayo katika dakika ya pili, ya nane na 53 na kuifanya Chelsea kushinda michezo yake mitatu ya mwanzo ya hatua ya makundi kwenye michuano ya vilabu Barani Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2010/2011 walipofanya hivyo kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya.
Mpaka sasa Chelsea haijapoteza mchezo wowote chini ya kocha Maurisio Sarri ambaye amesema lengo lake ni kufuzu hatua inayofuata mapema huku wakimaliza wakiwa vinara wa kundi lao.
Sarri ameongeza kuwa walicheza vema kwa dakika 65 na hakupenda waliporuhusu bao, kwa kuwa alitaka wamalize mchezo huo wakiwa hawajafungwa.
Kuhusu mchezo wao unaofuata wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Burnley, – Sarri amesema kuwa anajua utakuwa mgumu na huenda akafanya mabadiliko ya wachezaji sita mpaka saba kwani Burnley ni timu ngumu na ameshuhudia michezo yao mingi msimu uliopita, hivyo inawabidi kupamabana kupata matokeo.
Katika matokeo mengine ya michuano ya ligi ya Yuropa, mabao mawili ya nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, – Mbwana Samatta yametosha kuipa ushindi wa ugenini wa mabao manne kwa mawili timu yake ya Genk dhidi ya miamba ya Uturuki timu ya Besiktasi.
Samatta amefunga mabao hayo katika dakika za 23 na 70 kabla ya Diumerki Ndongala na Jakub Piotroski kuongeza mengine kwenye dakika za 81 na 83 huku mabao ya kufutia machozi kwa Besiktas yakifungwa na Sandro Vagner katika dakika za 74 na 86.
Mjini Milan, miamba ya Italia, – AC Milan wakiwa kwenye dimba la San Siro wamekubali kipigo cha mabao mawili kwa moja kutoka kwa Real Betis, Manyambizi wa Manyano Villareali wamesambaratisha Rapid Vien kwa kipigo kizito cha mabao matano kwa bila wakati Rangers wakishindwa kutamba nyumbani na kulazimishwa suluhu na Spartak Moscow.