Arsenal wameendeleza wimbi la ushindi baada ya usiku wa kuamkia leo kuweka rekodi ya kushinda mchezo wa 11 mfululizo katika mashindano yote kwa kuinyuka Sporting Lisborn ya Ureno bao moja kwa bila kwenye mchezo wa michunao ya Yuropa League.
Washika bunduki hao wa jiji la London wameendeleza rekodi hiyo ya ushindi tangu mwezi Oktoba mwaka 2007 waliposhinda michezo 12 mfululizo na ushindi wa jana unakuwa wa kwanza wa ugenini dhidi ya timu za Ureno baada ya kushindwa kushinda katika michezo sita iliyopita wakipoteza mitatu na kutoka sare mitatu.
Bao pekee kwa Arsenal limepachikwa kimiani na Danny Welbeck katika dakika ya 77 na kumfanya kuhusika kwenye mabao matano katika michezo mitano aliyoanza kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal kwa msimu huu katika mashindano yote.
Mchezo wa jana ni wa kwanza kwa Arsenal kucheza bila kuruhusu timu pinzani kupiga shuti hata moja lililolenga lango lao kwenye michuano ya Ulaya ambapo mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 2015 dhidi ya Monaco kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Barani Ulaya.
Katika hatua nyingine kocha wa kikosi hicho Unai Emery ameendelea kuwa mfalme wa michuano ya Yuropa akiweka rekodi ya kupoteza mchezo mmoja kati ya 21 ya hatua ya makundi kwenye michuano hiyo ambapo ameshinda michezo 12 huku akitoka sare katika michezo nane.