Rais Magufuli awataka viongozi kuridhika na nyadhifa zao

0
395

Rais John Magufuli amewataka viongozi mbalimbali aliowaapisha leo kwenda kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kutatua kero zinazowakabili ikiwemo migogoro mbalimbali ambayo inakwamisha juhudi za maendeleo ya wananchi hao.

Aidha, amewasihi viongozi wa Serikali kuridhika na nyadhifa walizonazo na kuelekeza nguvu zao kulitumikia Taifa badala ya kung’ang’ania kutaka nafasi zingine.

Amemtaka Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Gabriel Pascal Malata na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface Nalija Luhende kuhakikisha wanasimamia vizuri kesi zinazoihusu Serikali ili kulinda maslahi ya Taifa.

Pia, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt. Maduhu Isaac Kazi kuhakikisha TIC inavutia wawekezaji zaidi na inaondoa vikwazo dhidi ya wawekezaji wenye nia ya kuwekeza hapa nchini.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri wa TAMISEMI, Seleman Jafo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa.