Serikali ya Kenya imetangaza kuwa shule za msingi na shule za upili (sekondari) nchini humo zitaendelea kufungwa hadi mwaka 2021 kutoka na athari za janga la virusi vya corona.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Pof. George Magoha ambapo ameeleza kuwa wanafunzi wote wataendelea kukaa majumbani hata wale waliokuwa wamefikia kufanya mitihani ya taifa.
”Tulikuwa tumepanga wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha pili warudi shuleni lakini tumebadili wazo hilo,” amesema Magoha.
Kuhusu kufunguliwa kwa vyuo vya elimu ya juu, wizara hiyo imesema vitafunguliwa kwa awamu kwa sharti la kufuata kanuni zote za afya, na chuo chochote kitakachokiuka kanuni hizo kitafungwa.
Kenya imeendelea kushuhudia kasi ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona ambapo hadi leo Julai 7, 2020 jumla ya visa 8,067 vimerekodiwa chini humo.