Serikali yaagiza kuharakishwa kwa ujenzi wa Bandari ya Karema

0
288

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza kampuni ya Xiamen Ongoing Construction Group inayojenga bandari ya Karema kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 47, ifanye kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Karema inayojengwa kwenye ziwa Tanganyika katika kata ya Karema wilayani Tanganyika mkoani  Katavi.
 
Pia ametoa muda wa siku 21 kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi na Wizara ya Madini wawe wameanza kutoa huduma katika eneo la Ikola ili kuhudumia wageni wanaotoka katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
 
 Amesema mradi wa ujenzi wa bandari hiyo ya Karema una lengo la kuongeza tija katika shughuli za kibandari kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika na kwamba unatarajiwa kuongeza fursa za kibiashara na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.
 
“Tumeamua kujenga bandari hii ambayo itawezesha meli zaidi ya moja kupakia na kushusha abiria na mizigo kwa wakati mmoja, hii ni serikali ya kuahidi na kutekeleza na ni serikali ya kusikia na kutenda na ndio maana halisi ya falsafa ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Mradi huo wa ujenzi wa bandari ya Karema unatekelezwa kwa muda wa miezi 24 ukihusisha ujenzi wa gati kubwa la kufungia meli lenye urefu wa mita 150, ujenzi wa  kingo ya kuzuia mawimbi makali, uchimbaji wa kuongeza kina cha lango la kuingilia bandarini na sehemu ya kugeuzia meli.