Tanzania kuingia uchumi wa kati kutavutia wawekezaji

0
781

Serikali imewataka wananchi kuendelea kupenda bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini kwani chanzo cha nchi kufikia uchumi wa kati ni pamoja na wananchi wake kupendelea bidhaa ambazo wanazizalisha wao kama wao, na mafanikio yametokana na juhudi za watanzania wote wakiongozwa na Rais John Magufuli.

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (sabasaba) yanayofanyika  katika Viwanja vya Mwl. Nyerere Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Innocent Bashungwa amesema kuwa ili watanzania waweza kusheherekea mafanikio endelevu ya kuingia nchi zenye kipato cha kati wanatakiwa kuwa wa kwanza kutangaza bidhaa zao.

“Kupitia mafanikio tuliyoyapata rai yangu kwa Watanzania ni kupenda bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu ili mafanikio haya ya nchi kuwa kwenye orodha ya nchi zenye kipato cha kati yawe ni matunda kwa watanzania hasa kwa wakina mama na  vijana wanaotafuta ajira na tukiendelea kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ndivyo tunazidi kutengeneza fursa za ajira kwa watanzania,” amesema Bashungwa

Amesisitiza kuwa watanzania wanatakiwa kuangalia bidhaa za ndani Kabla hawajanunua bidhaa kutoka nje ili kuweza kukuza viwanda na kuwa na uchumi wenye kipato cha kati endelevu kwani ili Watanzania waendelea kusheherekea mafanikio haya ya kufikia kipato cha kati tunatakiwa kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Amebainisha kuwa kupitia maonesho 44 ya Biashara kimataifa (sabasaba)  ambapo kampuni mbalimbali ndani na nje ya nchi zitashiriki, kutakuwa na fursa ya wananchi kuja kununua bidhaa na kuangalia teknolojia mbalimbali zikioneshwa na taasisi na makampuni ya kitanzania,  pia kupitia B2B wale ambao wapo nje wataendelea kuingia mikataba na wafanyabiashara ambao wanashiriki katika maonesho ya sabasaba hayo.

Pamoja na hayo Bashungwa amesema Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati inasaidia kuingia kwenye rada ya kimataifa hivyo wengi watapenda kuja kuwekeza hapa nchini.