Ndugu wafukua mwili wa marehemu kuufanyia uchunguzi

0
233

Mwili wa mkazi wa Chimala wilayani Mbarali umefukuliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya kufuatia ndugu wa marehemu kuwa na utata wa kifo chake kilichotokea mapema mwezi wa tatu mwaka huu kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ulrich Matei amesema wamefikia hatua hiyo ya kufukua mwili wa Tulizo Konga baada ya ndugu wa marehemu kutaka ufanyike uchunguzi wa kina juu ya kifo cha ndugu yao.

Ashel Konga ni baba mzazi wa marehemu, anasema familia imefikia hatua ya kufukua kaburi kutokana na kwamba wakati wa mazishi hawakushirikishwa, ndipo wakaenda kituo cha polisi kuomba kibali cha kufukua kaburi ili kuhakikisha kama ni kweli ni ndugu yao na kujua chanzo cha kifo chake.

Dada wa marehemu Salome Konga, amesema amefurahishwa na kitendo cha jeshi la polisi kuwaruhusu kufukua kaburi hilo na kutambua mwili wa mpendwa wao ambaye alifariki katika mazingira ya kutatanisha licha ya kukumbana na changamoto nyingi kufikia hatua hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amezungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo na kutoa ufafanuzi wa tukio.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi mkoa wa mbeya linamshikilia Joseph Shiba(29) ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Mwakaleli halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe kwa tuhuma za wizi wa shilingi milioni thelathini nane za mwalimu mstaafu, Gidion Mwalujobho (60) mkazi wa Mwakaleli.