Watu wanne wamepoteza maisha na wengine 27 kujeruhiwa baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria katika Ziwa Victoria wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kupigwa na radi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa Mwanza, Muliro Jumanne mtumbwi wenye jina la One Ten ulipigwa na radi ukiwa safarini kati ya eneo la Kome na Buganda, Kata ya Bukiko.
Watu wanne waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni nahodha wa mtumbwi, Kumunya Andrea na msaidizi wake Simon Charles pamoja na abiria wawili Deogratius Mulungu na Ndege Abdu.
Majeruhi 27 wa ajali hiyo wamelazwa katika Zahanati ya Bukiko pamoja na Kituo cha Afya Bwisya.
Aidha, katika tukio jingine, kijjini Mwampuru, wilayani Kwimba mtoto Dalaile Milambo (6) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na fisi katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Jumanne amesema polisi kwa kushirikiana na idara ya wanyamapori pamoja na wananchi hicho wanaendelea kumsaka fisi huyo ili aweze kudhibitiwa kwa mujibu wa sheria kabla hajasababisha madhara zaidi.