Wizara yaagiza kuundwa kamati ya kutatua changamoto za ardhi

0
201

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefanya ziara katika Kiwanda cha Saruji cha Maweni kilichopo jijini Tanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kutatua kero mbalimbali.

Akielezea changamoto zilizopo katika kiwanda hicho Meneja Mkuu, James Jing amesema kumekuwepo na changamoto ya upatikanaji wa haki ya kumiliki ardhi (surface right) kutoka kwa wamiliki wa ardhi hali inayopelekea kukwama kwenye maombi ya kuhuisha leseni za madini na kufanyiwa tathmini ya mazingira.

Naibu Waziri Nyongo ameelekeza kuundwa kwa kamati itakayojumuisha wajumbe kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Tume ya Madini, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa ajili ya kukaa pamoja na kutatua changamoto hiyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo amewahakikishia wamiliki wa kiwanda hicho kuwa Serikali itahakikisha changamoto husika inatatuliwa na kuanza shughuli za uzalishaji mara moja na kulipa kodi mbalimbali Serikalini.

Na Bertha Mwambela Tanga