Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameziataka ofisi za ardhi za mikoa zilizozanzishwa hivi karibuni kuwa na daftari maalum lenye orodha ya migogoro ya ardhi ili kurahisisha ufuatiliaji sambamba na utatuzi wa migogoro kwenye mikoa.
‘’Sasa hivi hatutegemei migogoro mipya maana migogoro tunayoshughulika nayo sasa ni ile ya miaka ya nyuma hivyo muorodheshe migogoro yote iliyopo wilayani na kuanza kuishughulikia,’’ amesema Lukuvi.
Waziri Lukuvi ameshangazwa na ofisi za ardhi katika halmashauri za wilaya nchini kushindwa kutatua migogoro ya mipaka baina ya wilaya na wilaya wakati halmashauri hizo zina wataalamu wa sekta ya ardhi wanaoweza kuitafsiri GN.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika ukaguzi wa mashamba makubwa yaliyomilikishwa kwa wawekezaji kwenye mkoa wa Manyara ili kubaini mashamba yasiyoendelezwa.
Hatua hiyo inafuatia kuelezwa na Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexzander Mnyeti kuwa, mkoa huo una mashamba makubwa yasiyoendelezwa kwa muda mrefu wakati uhitaji wa mashamba kwa wananchi wa mkoa huo ni mkubwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu.
‘’Hatujatoa ardhi kwa ajili ya kuweka akiba, kazi ya ukaguzi mashamba ni ya kwenu hivyo myaangalie kama yameendelezwa, yana faida gani na yanalipa kodi,” amesema Waziri Lukuvi.