Serikali leo imekabidhiwa mawe mawili makubwa ya madini ya Tanzanite yaliyochimbwa na mchimbaji mdogo, Saniniu Laizer.
Madini hayo yamekabidhiwa huko Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa Waziri wa Madini Doto Biteko kwa niaba ya serikali ambapo ametoa wito kwa watendaji kuwasaidia wachimbaji wadogo katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kuwa Rais John Magufuli ameagiza mawe hayo yenye uzito wa takribani kilo 14 yanunuliwe na serikali na mchimbaji huyo mdogo asidhulumiwe chochote anachostahili.
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Madini, mawe hayo yamenunuliwa na serikali kwa shilingi bilioni 7.74 na kwamba yatawekwa katika makumbusho.
Hii ni mara ya kwanza kwa kiasi hicho kikubwa cha madini ya Tanzanite kuchimbwa tangu uchimbaji wa madini hayo uanze.