Malawi wapiga kura mara ya pili kumchagua Rais

0
655

Raia wa Malawi leo Juni 23 wamerejea tena katika vituo vya kupiga kura kumchagua Rais wa nchi hiyo baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2019 kubatilishwa na Mahakama ya Katiba.

Mwezi wa Februari mwaka huu, mahakama hiyo iliamuru uchaguzi huo ufanyike tena baada ya kutoa hukumu kwamba matokeo ya uchaguzi wa kwanza yaliyompa ushindi Rais Peter Mutharika yalikuwa batili kutokana na ushahidi uliobainisha kasoro kadhaa na udanganyifu katika hesabu za kura.

Zaidi ya vituo 5,000 vinatumiwa na raia milioni 6.8 wa Malawi wenye sifa za kupiga kupiga kura katika kutekeleza haki yao ya msingi ya kidemokrasia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amewataka viongozi wa kisiasa nchini Malawi na wadau wengine wote wa siasa kuhakikisha uchaguzi huo wa Rais unafanyika katika mazingira ya amani.