Serikali imeitaka jamii kuhakikisha watoto wanapata chanjo kipindi hichi chenye maambukizi ya Virusi vya Corona (Covid-19) ili wapate kinga ya magonjwa mengine.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto, Dkt. Ahmad Makuwani kwenye semina ya waandishi wa habari wa Mikoa ya Singida na Dodoma kuhusu huduma za chanjo nchini.
Amesema maambukizi ya Corona kwasasa yamepungua na kuwataka watanzania kutotumia ugonjwa huo kama sababu ya kutowapeleka watoto kupata chanjo.
“Tulikuwa tunaenda vizuri lakini hivi karibuni idadi ya watoto na wasichana wanaopaswa kupata chanjo ya mlango wa kizazi imepungua, hizi chanjo ni muhimu sana jamii ipeleke watoto kwenye vituo wapate chanjo” amesema Dkt. Makuwani.
Amebainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kwasasa katika utoaji wa huduma za chanjo huku akieleza kuwa kuna vituo zaidi ya 600 vinavyofanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.
“Tunaamini mtatumia weledi wenu kuelimisha jamii kuhusu huduma ya chanjo mbalimbali zinazotolewa, wahimizeni wananchi kule vijijini wapeleke watoto wao kwa kuwa chanjo inatolewa kwenye vituo vya kutolea huduma” amesema Dkt Makuwani.
Awali, akizungumzia hali ya huduma za chanjo nchini, Ofisa Programu ya Chanjo wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Lotalis Gadau, amesema pamoja na jitihada za kuhakikisha magonjwa yanayizuilika kwa chanjo yanapewa kipaumbele kwa kuwapatia watoto chanjo lakini bado kuna jamii hazichanji watoto.
“Baadhi ya chanjo kiwango kipo chini ya kiwango kinachotakiwa, chanjo ya Surau na Rubella kitaifa tuna asilimia 76% ambayo iko chini ya kiwango cha utoaji wa huduma za chanjo ambayo inatakiwa kuwa asilimia 90” amesema Bi. Gadau kupitia tathmini ambazo hufanywa na wizara kuona hali ya huduma za chanjo.
Amesema kuwa Wizara imekuwa ikifanya usimamizi elekezi wa huduma za chanjo katika kipindi ambacho mlipuko wa ugonjwa wa corona ulivyoanza na shule kufungwa kuona hali ya utoaji wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwenye jamii ambapo wananchi wengi wamekuwa wakiogopa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakiogopa maambukizi na kuihamasisha jamii kwenda kupeleka watoto wao kupata chanjo hizo muhimu huku wakizingatia tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa corona.