Jeshi la Wananchi wa Tanzania limetuma timu ya wataalamu kwenda kutoa lori la mizigo ambalo limetumbukia katika Daraja la Mto Wami kwa zaidi ya wiki moja na kushindikana kutolewa .
Kiongozi wa timu hiyo Kapteni Obed Mwakalobo kutoka Kikosi cha Nyumbu amemwambia Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa kwamba kazi ya kutoa lori hilo imeshaanza na wanatarajia ifikapo kesho iwe imekamilika.
Amesema kwa sasa wataalamu hao tayari pamoja na wazamiaji wameshawasili katika eneo lilikotumbukia lori hilo na wameshaanza kuzamia ndani ya maji kuangalia namna ambavyo lori hilo litakavyotolewa.
Kwa upande wake mmiliki wa lori hilo Mwajuma Selemani ameishukuru serikali kwa kutuma wataalamu hao wa jeshi kwenda kusaidia kutoa lori hilo.
Kwandikwa amesema serikali itasimamia zoezi hilo pamoja na kulifanyia maboresho daraja hilo ili liendelee kutumuka hadi hapo mradi wa ujenzi wa daraja jipya katika mto huo utakapokamilika.