Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wanachama wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali za uwakilishi wa wananchi kuwa na maono yanayofanana na ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli yenye kujali na kuwatumikia wananchi.
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Humprey Polepole amesema hayo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari na kubainisha kuwa, chama hicho hakitaruhusu wagombea wenye mlengo wa maslahi binafsi.
Amesema mchakato wa uchukuaji fomu kuwania nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ule wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar utaanza Juni 15 na kumalizika June 30 mwaka huu na kwa nafasi za Ubunge na Uwakilisha ratiba itatangazwa hapo baadae.
Aidha Polepole amesisitiza kuwa mwanachama yoyote atakayejihusisha na viashiria vya rushwa atapoteza sifa ya kugombea nafasi ya uongozi na kwamba ataripotiwa kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).