Vigogo 69 wa CHADEMA kuhojiwa TAKUKURU sakata la matumizi ya fedha

0
441

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema imewaita kwa ajili ya mahojiano wabunge na waliowahi kuwa wabunge kupitia chama hicho, ambao jumla ya wote ni 69, kwa ajili ya mahojiano.

Taasisi hiyo imesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za chama zilizotolewa na baadhi ya wabunge hivi karibuni.

TAKUKURU imeeleza kuwa inafanya uchunguzi wa jambo hilo kwa sababu ndani yake kunaweza kukawa na makosa ya ubadhirifu wa fedha za chama na matumizi mabaya ya madaraka, makosa ambayo yanaangukia kwenye mamlaka yake.

Baadhi ya wabunge wa chama hicho walilalamikia makato ambayo yamekuwa yakifanywa kwenye malipo yao, ambapo wabunge wa viti maalum wamekuwa wakikatwa TZS milioni 1.56, huku wabunge wenye majimbo wakikatwa TZS 520,000 kwa mwezi.

Wakati huo huo, TAKUKURU Mkoa wa Morogoro inamchunguza aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho, Dkt. Christine Ishengoma kwa tuhuma za kuhusika katika vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu.

Taasisi hiyo pia inakusudia kumkamata aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Boma, Amiri Nondo na wenzake watatu wanaotuhumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi.