Kongamano la kimataifa la uwekezaji laendelea Uswisi

0
1970

Tanzania ni  miongoni mwa nchi 160 duniani zinazoshiriki katika kongamano la kimataifa la uwekezaji (World Investment Forum) linaloendelea Geneva, -Uswisi.

Kongamano hilo la siku Tano limebeba kaulimbiu inayosema kuwa uwekezaji kwa maendeleo endelevu na lina lengo la kuimarisha uwekezaji kwenye nchi hizo.

Pamoja na mambo mengine, washiriki wa kongamano hilo lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) wanajadili changamoto za uwekezaji katika mazingira mapya ya utandawazi na mapinduzi ya viwanda.

Kongamano hilo limekua likiandaliwa na UNCTAD kila baada ya miaka miwili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya uwekezaji ambapo kwa mwaka huu kuna zaidi ya  washiriki elfu Tano kutoka nchi hizo 160 duniani ambapo ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Dkt. James Msekela.

Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC)  nacho kinashiriki katika kongamano hilo ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho  Geoffrey Mwambe anashiriki katika vipindi, midahalo na majadiliano mbalimbali kwa lengo la kuinadi Tanzania hasa  katika  fursa za uwekezaji.