CHADEMA yajitosa kinyang’anyiro cha Urais Zanzibar

0
247
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Zanzibar), Salum Mwalimu akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Kisiwandui, Unguja, kuhusu maandalizi ya CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu visiwani humo.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa upande wa Zanzibar kimetangaza kushiriki kugombea nafasi ya Urais wa Zanziabar katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu.

Akitangaza uamuzi huo mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA kwa upande wa Zanzibar, -Salum Mwalimu amewataka wanachama wa chama hicho wenye sifa na maadili kujitokeza na kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.

Amesema Mwanachama yeyote mwenye nia ya kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar kuanzia leo anaweza kupeleka barua ya maombi katika mamlaka zinazohusika ndani ya CHADEMA na kwamba zeozi hilo la siku kumi litafika tamati Juni 16 mwaka huu.

Mwalimu ameongeza kuwa milango ipo wazi kwa mwanachama yeyote wa CHADEMA mwenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Hivi karibuni akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa CHADEMA Taifa John Mnyika alitangaza kuwa chama hicho kimefungua milango kwa Mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho.