Marekani yaonywa kufuatia mauaji ya raia wake wenye asili ya Afrika

0
605

Umoja wa Mataifa umelaani mauaji ya raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika,- George Floyd yaliyotokea mikononi mwa polisi hivi karibuni.

Katika taarifa yake Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameitaka serikali ya Marekani kudhibiti mauaji ya raia wa Taifa wenye asili ya Afrika wasio na silaha.

Amesema mauaji ya Floyd ni miongoni mwa mauaji mengi ya watu wa aina hiyo nchini Marekani, hivyo ni lazima yakomeshwe mara moja.

Katika taarifa yake Bachelet pia ameelezea mauaji ya Ahmaud Arbery na Trayvon Martin ambao pia ni raia wa Marekani wenye asili ya Afrika ambao nao waliuawa katika matukio yanayofanana na lile la Floyd.

Mwanzoni mwa wiki hii George Floyd aliyekua na umri wa miaka 46 na mfanyakazi kwenye mgahawa mmoja nchini humo aliuawa akiwa katika mikono ya polisi mjini Minneapolis.

Mauaji hayo yamezusha maandamano katika maeneo mbalimbali nchini Marekani hasa baada picha ya video iliyerekodiwa na mpita njia kuonesha namna polisi mzungu alivyokuwa akitumia goti kumkandamiza shingoni Floyd aliyefungwa pingu huku akiomba msaada kutokana na kukosa pumzi.