Corona: Wananchi wa Uganda waruhusiwa kuanza kutoka nje

0
416

Serikali ya Uganda leo itaanza kulegeza masharti ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, ambapo magari binafsi yataruhusiwa kurejea barabarani, huku maduka na migahawa kufunguliwa.

Licha ya masharti hayo kuanza kulegezwa, serikali imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo vinavyosababishwa homa ya mapafu (Covid-19).

Rais Yoweri Museveni amesema kuwa ni lazima watu wote kuvaa barakoa watokapo majumbani mwao, na serikali imeahidi kugawa barakoa hizo bure kwa watu wenye umri kuanzia miaka sita.

Hata hivyo, masharti hayo yatalegezwa kwanza kwenye wilaya 95 kati ya wilaya 135, huku wilaya 40 zilizopo mipakani zikiendelea na mashrti ya kubaki ndani.

Sehemu za mazoezi (gyms), kumbi za starehe (night clubs) zitaendelea kufungwa, huku usafiri wa umma ukitarajiwa kuanza kutumika Juni 4, siku ambayo muongozo wa kufungua shule utakapotolewa.