Watuhumiwa saba wa ujambazi wauawa

0
212

Watu Saba wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa katika majibizani ya risasi na askari polisi katika eneo la Mwenge jijini Dar es salaam.

Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, -Lazaro Mambosasa amewaambia waandishi wa habari kuwa mbali na kuuawa kwa watuhumiwa hao wa ujambazi, polisi pia wamekamata bastola aina ya Bereta ikiwa na risasi tatu ndani ya kasha.

Amesema tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku wa kuamkia hii leo ambapo watu hao wakiwa ndani ya gari namba T 956 BYA Toyota Noah, wanadaiwa walikua wakielekea kufanya uhalifu katika ghala la GS Group Limited linalohifadhi vifaa vya pikipiki.

Kamanda Mambosasa amesema Polisi wa Kanda Maalum Dar es salaam walipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuhusu njama za watu hao na kufika eneo la Mwenge Coca cola, na walipojaribu kulifuata gari hilo liliongeza mwendo na kuchepuka barabara ya vumbi na ghafla watu hao walianza kulishambulia gari la polisi kwa risasi.

Vitu vingine vilivyokutwa ndani ya gari la watuhumiwa hao wa ujambazi ni pamoja na mitungi miwili ya gesi na mipira yake, mapanga matatu na kamba za katani.