Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amewataka madereva wa malori nchini kuhakikisha wanakula vyakula ambavyo vitalinda kinga zao za mwili.
Waziri Ummy Mwalimu ametoa rai hiyo na kuwataka madereva kuendelea kuchukua tahadhari za Corona wakati akizungumza na baadhi ya madereva wa kampuni mbalimbali za malori zinazosafirisha mizigo nje ya nchi waliofika katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko Mabibo, Dar es Salam kwa ajili ya kupima kama wana maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona au
“Nimefurahi sana kuwaona mko hapa kwa ajili ya kupima virusi vya Corona kama mtakutwa hamna maambukizi ya ugonjwa huu mjitahidi kula matunda yakiwemo machungwa, mananasi, malimao, mboga za majani na tangawizi hii itawasaidia kinga zenu za mwili kuwa juu. Pia muwapo safarini mnapopata nafasi msisahau kupiga nyungu,” amesema waziri Mwalimu.
Mwalimu amesema ugonjwa wa Corona bado upo ingawa maambukizi yamepungua jambo la muhimu ni kwa wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya hii ikiwa ni pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, kuvaa barakoa pia kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa maabara ya Taifa ya afya ya jamii Ambele Mwafulango amesema, kwa upande wa madereva walioko jijini Dar es Salaam kwa siku wanawapima madereva 200, kwa madereva walioko mikoani kuna utaratibu maalum wa kuchukuliwa sampuli ambazo zinatumwa Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo.
Majibu ya vipimo hivyo yanatoka baada ya masaa 48 kama madereva hao watakutwa hawana maambukzi watapewa vyeti ambavyo vinatumika kwa siku 14 hii itawasaidia kwenda kupeleka mizigo nje ya nchi bila ya kupimwa tena katika nchi wanazokwenda.
Mwafulango alisema kabla madereva hao hawajafanyiwa vipimo vya Corona wanapimwa joto la mwili na wale ambao watakutwa na joto la juu la mwili watapewa huduma ya haraka zaidi ukilinganisha na wale ambao joto lao la mwili liko sawa.
“Madereva ambao tunawakuta hawana maambukizi ya ugonjwa wa Corona tunawapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu wanapokuwa safarini siku zote.
“Katika maabara hii ya Mabibo tuna mashine mpya tano ambazo ndani ya masaa 24 zinapima vipimo 1800 hii imetufanya kupima vipimo vingi zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa katika maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za NIMR jijini Dar es Salaam ambapo tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinapima vipimo 300 hadi 400 jambo ambalo lilikuwa linachelewesha utendaji wetu wa kazi,” amesema Mwafulango.