Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema idadi ya wagonjwa wa corona imeendelea kupungua huku baadhi ya vituo vikiwa havina wagonjwa.
Akizungumza mara baada ya sala ya Idd El Fitri katika msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema, licha ya wagonjwa kupungua bado hatua za kujikinga zinapaswa kuchukuliwa ili ugonjwa uendelee kupungu.
“Kwa mujibu wa takwimu za leo asubuhi Dar es Salaam kuna wagonjwa 11, Kibaha 16 na Dodoma kituo cha Mkonze wagonjwa ni watatu” amesema Majaliwa
Amesema, takwimu kuonyesha maambukizi kushuka ni nzuri lakini jambo kubwa kwa sasa ni kuendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia uwezekano wa mtu kuambukiza na kuambukizwa huku akiwataka wananchi kuendelee kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wataalam wa Afya.
“Naomba tuendelee kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na njia zote zinazozuia maambukizi kutoka mtu mmoja hadi mwingine” amesema Waziri Majaliwa