Rais John Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa mitano nchini ambayo iko katika maeneo ya mpaka wa Tanzania na Kenya pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe kukutana na wenzao wa Kenya ili kutatua mgogoro ambao umeonekana kujitokeza katika siku za hivi karibuni.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa mkoa wa Singida na kuongeza kuwa mgogoro huo ambao umejitokeza katika maeneo ya mipakani baada ya madereva kuzuiwa kuingia katika nchi hizo kutokana na hofu ya maambukizi ya corona ni lazima umalizwe.
Amesisitiza kuwa Tanzania na Kenya ni marafiki na ndugu, hivyo virusi vya corona haviwezi kudhoofisha urafiki huo.
Rais Magufuli amesema yeye pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wameishamaliza jambo hilo na kwamba anataka mgogoro huo umalizike kabisa hata kwa viongozi wa ngazi ya chini.
Hivi karibuni madereva wa magari kutoka nchini Tanzania walizuiliwa kuingia nchini Kenya, hali iliyosababisha mamlaka kwa upande wa Tanzania nazo kuwazuia baadhi ya madereva wa magari kutoka Kenya kuingia nchini.