Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigella ameziagiza mamlaka zote zilizopo katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga kutoruhusu lolote kuingia nchini kutoka nchini Kenya.
Shigella ametoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea eneo hilo na kukuta baadhi ya madereva wa Kitanzania wakiwa katika eneo hilo kwa zaidi ya siku sita bila ya kuruhusiwa kuingia upande wa Kenya.
Amesema kwa magari yoyote yanayotoka nchi za Rwanda na Burundi yaruhusiwe kupita katika mpaka huo wa Horohoro kwa kufuata taratibu zilizopo.
Aidha ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mpaka huo ili kuzuia watu wanaoingia nchini kinyume cha sheria.