Watakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi ndani ya siku 14

0
444

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinapeleka hati za madai ya kodi ya pango la ardhi kwa wadaiwa sugu wa kodi hiyo kuanzia hii leo, na watakaokaidi kulipa kwa hiari wafikishwe kwenye mabaraza ya ardhi ya nyumba ya wilaya.

Agizo hilo limetolewa mkoani Iringa na naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula akiwa katika ziara yake mkoani humo kwa lengo la kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika baadhi ya taasisi za mkoa huo.

Amezitaka idara za ardhi katika halmashauri zote nchini kupitia kumbukumbu za wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi vizuri na kuwaandikia hati za madai zitakazowataka kulipa kwa hiari madeni yao.

“Wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi baada ya hati ya madai kupelekwa wawe wamelipa kodi hiyo kwa hiari ndani ya siku kumi na nne na wakishindwa wafikishwe kwenye mabaraza ya ardhi ya nyumba ya wilaya, tunataka ikifika juni 30 mwaka huu wizara iwe imekamilisha kukusanya shilingi bilioni 180 kama ilivyojiwekea katika malengo yake’’ amesisitiza naibu waziri Mabula.

Akiwa katika ziara yake, Dkt Mabula amekutana na wadaiwa sugu wa mkoa wa Iringa  ambao ni pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka mkoa wa Iringa (IRUWASA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Iringa, Benki ya CRDB na kituo cha Radio cha EBONY ambao kwa pamoja wanadaiwa zaidi ya shilingi milioni 128.