Kauli ya JPM yawapa matumaini wafanyabiashara wa vitu asili

0
234

Wafanyabiashara wa soko la vitu vya asili la Masai Market lililopo jijini Arusha wamesema wana matumaini ya biashara yao kurejea kama awali, kufuatia kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati aliposhiriki Ibada ya jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Chato mkoani Geita.

Wakizungumza na Mwandishi wa TBC mkoani Arusha, wafanyabishara hao wamesema kauli ya Rais Magufuli kuwa kuna idadi kubwa ya watalii kutoka nje wanataka kuja nchini ni njema kwao, kwa kuwa watalii ndio tegemeo kubwa katika soko hilo.

Wamedai kuwa walikuwa wamefunga biashara zao kwa muda mrefu kutokana tishio la virusi vya corona, hali iliyozilazimu nchi mbalimbali duniani kusitisha safari za nje.

Akizungumza wakati wa Ibada hiyo, Rais Magufuli alisema kuwa watalii wengi wameonesha nia ya kukata tiketi za kuja nchini, hivyo ameiagiza wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mamlaka zingine zinazohusika kutowazuia watalii na ndege zinazotaka kuleta wageni nchini.