Mawakala wa utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wapo katika kisiwa cha Mafia mkoani Pwani kwa lengo la kuangalia vivutio vya utalii vinavyopatikana katika kisiwa hicho.
Wakiwa katika kisiwa hicho cha Mafia, Mawakala hao pamoja na mambo mengine wataishauri Bodi ya Utalii Nchini (TTB) namna ya kuweka mpango maalumu wa kutangaza vivutio hivyo vya utalii ambavyo baadhi yake havipatikani mahali popote Barani Afrika isipokuwa Mafia pekee.
Mawakala hao wameyataja maeneo ambayo yakitangazwa vizuri yanaweza kuvutia watalii wengi kutembelea kisiwa cha Mafia kuwa ni ni pamoja na lile analopatikana samaki mkubwa aina ya Potwe ambaye katika Bara la Afrika hupatikana katika kisiwa hicho cha Mafia peke yake.
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya bahari Dkt Jean de Villiers amesema kuwa samaki aina ya Potwe ni kivutio kikubwa kinachopendwa kuonwa na watalii wengi, hivyo ni wajibu wa Bodi ya Utalii Nchini kuona kivutio hicho kama fursa pekee inayoweza kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea kisiwa cha Mafia na kuchangia pato la Taifa.
Kwa mujibu wa Bodi hiyo ya Utalii Nchini, mafanikio makubwa yanatarajiwa kupatikana baada ya Mawakala hao wa utalii kutoka mataifa mbalimbali duniani kutembelea maeneo matano makubwa yenye vivutio vikubwa vya utalii nchini kikiwemo kisiwa cha Mafia na Zanzibar.