Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) tayari imetenga shilingi bilioni 1.2 kwaajili ya kujenga laini ya kusafirisha umeme mkubwa yenye urefu wa takribani kilomita 100 ambayo itakuwa ni maalumu kwaajili ya Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa pekee.
Amesema hayo wakati akizuru kiwandani hapo na kuangalia upatikanaji wa umeme katika kiwanda hicho kikubwa cha kuzalisha sukari kilichopo Morogoro.
Hata hivyo, Kalemani amesema kuwa, mahitaji ya umeme katika kiwanda hicho kwa sasa ni megawati 5 mpaka 8 lakini kutokana na maboresho makubwa ambayo yameelezwa kufanyika kiwandani hapo ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Waziri Kalemani ameongeza kuwa ujenzi wa laini hiyo utakwenda sambamba na ongezeko la kiasi cha umeme ambacho kitafikishwa kiwandani hapo ikiwa ni megawati 27 mpaka 40, ili kukidhi ongezeko la mahitaji yoyote ya umeme yatakayojitokeza kiwandani hapo ndani ya miaka mitano mpaka kumi ijayo.
Ujenzi wa maboresho hayo unatarajiwa kuanza haraka ndani ya siku mbili zijazo.