Watuhumiwa wanne wa ujambazi wauawa Kigoma

0
235

Watu wanne wanaosadikiwa kuwa Majambazi wameuawa baada ya kurushiana risasi na Askari Polisi katika kijiji cha Mvugwe wilayani Kasulu, Kigoma.

Askari wamefanikiwa kukamata risasi 153 na bunduki moja aina ya SMG.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma Martin Otieno, amesema katika muendelezo wa operesheni ya kusaka majambazi, jeshi hilo limefanikiwa kukamata watu wengine wanne wakiwemo wanawake wawili na bunduki moja ya kivita aina ya AK47 ikiwa na risasi arobaini na tisa.

Kamanda Otieno ametaja watu waliokamatwa ikiwa ni pamoja na Yoram Hamisi, Abel Ngoma, Kalesi Yoram na Asha Hamisi wote wakazi wa Kasulu.

Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta Ally Hamisi anayetuhumiwa kuwa ndio muhusika mkuu wa matukio ya ujambazi mkoani humo na kumtaka ajisalimishe popote pale alipo.

Aidha katika hatua nyingine, jeshi hilo limefanikiwa kukamata bunduki 27 aina ya gobore na silaha 3 za jadi zilizokuwa zikitumika katika uwindaji haramu na watu watatu kukamatwa baada ya kukutwa na vipande vinne vya pembe za ndovu.

Otieno amewataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uwepo wa viashiria vya ujambazi katika maeneo yao.