Serikali yasema dawa ya corona si ya kugawa kwa wananchi

0
673

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema kuwa dawa za kukabiliana na virusi vya corona ambazo Tanzania imepokea kutoka nchini Madagascar hazitogawiwa kwa wananchi kwa sasa.

Akizungumza katika hafla ya upokeaji wa dawa hizo hapa nchini, Prof. Palamagamba kabudi amebainisha kuwa dawa hizo zitafanyiwa utafiti kwanza, na zitakapothibitika kuwa zina faa, ndipo wananchi wataanza kutumia.

“Dawa hii tumepewa na Madagascar ili tuje tuifanyie utafiti kabla ya kuitumia. Tungekuwa tumeenda kuchukua dawa kwa ajili ya Watanzania wote tungeenda na Bombardier au Airbus, lakini tulienda na ndege ya Rais. Na ieleweka hatukwenda kuchukua kikombe cha babu,” amesema Kabudi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Prof. Abel Makubi amebainisha kuwa katika uchunguzi utakaofanyika, watalaangalia kama dawa hiyo ni salama kutumiwa, na pia ubora wake katika kupambana na corona.

Ameongeza kuwa nchini Madagascar tayari wamefanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa dawa hiyo inafaa ndio maana wameanza kutumia.

Pia amesisitiza kwa mara nyingine kwamba ieleweke kwamba dawa hiyo haikuletwa kwa ajili ya kugawiwa kwa watu.