Mvua zaleta maafa Mara, baadhi wakimbia makazi yao

0
418

Wakati mvua zikiendela kunyesha maeneo mbalimbali nchini, zaidi ya nyumba 40 katika mtaa wa Kitaji-D, Manispaa ya Musoma mkoani Mara zimezungukwa na maji.

Hali hiyo imewalazimu baadhi ya wakazi wa nyumba hizo kuyahama makazi yao kwa muda.

Nyumba hizo ambazo zipo jirani na Ziwa Victoria zimezingirwa na maji kufuatia kuongezeka kwa maji katika ziwa hilo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, hasa mkoani Mara.

Wakizungumza na TBC, baadhi ya wakazi hao pamoja na Diwani wa Kata hiyo, Frank Wabare wameiomba Serikali kuona namna ya kuweza kuwasaidia kwani wameshindwa kuhama kutoka katika maeneo hayo kutokana na ugumu wa maisha.

Wakati hali ikiwa hivyo mkoani Mara, baadhi ya wakazi wa Moshi, Kilimanjaro kata ya Rau waliokumbwa na mafuriko wameiomba serikali kuwapatia msaada wa vitu muhimu, kwani sehemu kubwa ya mali zao ilisombwa na maji.

Pia wameomba kujengewa Daraja la Mto Rau ambalo limegeuka kuwa tatizo sugu.