Huku Dunia ikiendelea kukabiliana na janga la virusi vya corona, Marekani imetangaza kuanza kutoa dawa mpya inayolenga kusaidia waathirika wa ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19).
Hatua hiyo imefikiwa baada ya dawa ya Remdesivir inayotumika kutibu ebola, kuonesha mafanikio makubwa kwa watu walioathiriwa na virusi vya Corona.
Dawa hiyo imeonesha kuwasaidia waathirika wa corona kwa kupunguza muda ambao dalili zinaonekana kutoka siku 15 hadi siku 11.
Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa dawa hiyo itatolewa kwa watu milioni 1.5 na kusambazwa katika hospitali mbalimbali nchini humo.
Hata hivyo wataalamu wamesema kuidhinishwa kwa dawa hiyo siyo mwisho wa kuendelea na tafiti za kusaka dawa ya corona, kwani bado hakuna ushahidi kwamba Remdesivir inauwezo wa kuponyesha wagonjwa wa corona.